Rais William Ruto amesema kuwa serikali itawekeza shilingi bilioni 9.5 kuimarisha uchumi wa baharini katika Ziwa Victoria.
Akizungumza leo Jumanne katika kaunti ya Siaya alipozindua upanuzi wa ufuo wa Usenge Pier utakaogharimu shilingi bilioni moja, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa mradi huo utasaidia kubuni nafasi za ajira na kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Kulingana na Rais Ruto, mradi huo wa Usenge Pier, unalenga kubadilisha sekta ya uvuvi, kuboresha maisha ya wenyeji na kupiga jeki ukuaji wa uchumi.
Aidha, Rais alisema mradi huo pia unalenga kuongeza mchango wa uchumi wa baharini kwa mapato ya taifa akiongeza kuwa miundombinu iliyoboreshwa itafanikisha usalama wa majini na kupunguza matukio ya ajali kwenye Ziwa Viktoria.
“Tutajenga kituo cha dharura cha wavuvi katika kaunti ya Siaya kwa shilingi milioni 250, tutanunua mashua za shughuli za uokoaji kwa shilingi milioni 70 na shilingi zingine milioni 70 zitumike kuimarisha ufugaji na kuongeza uzalishaji wa samaki,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto yuko kwenye ziara ya maendeleo katika eneo la Nyanza.