Serikali itaanzisha mpango wa utoaji chanjo kwa mifugo kote nchini mwezi Januari mwakani.
Hayo yamesemwa na Rais William Ruto.
Amedokeza kuwa wakati wa mpango huo, ng’ombe milioni 22 na mbuzi na kondoo milioni 50 watachanjwa.
Rais ameelezea kuwa mpango huo utasaidia kuzuia magonjwa ya mifugo na hivyo kupata soko la kimataifa kwa ajili ya bidhaa za mifugo.
“Hii itahakikisha upatikanaji wa masoko ya kitaifa na kimataifa kwa ajili ya bidhaa zetu za mifugo,” amesema Ruto.
Aliyasema hayo wakati Tamasha la Kitamaduni la Maa lililofanyika karibu na Hifadhi ya Kitaifa ya Samburu katika kaunti ya Samburu leo Ijumaa.
Miongoni mwa waliohudhuria tamasha hilo ni Waziri wa Utalii Rebecca Miano, Magavana Jonathan Lati Lelelit (Samburu), Patrick ole Ntutu (Narok), Joseph ole Lenku (Kajiado) na Mohamud Ali (Marsabit).
Ni wakati wa hafla hiyo ambapo Rais Ruto alisema serikali imetenga shilingi bilioni moja za ununuzi wa mifugo ili kujaza pengo lililoachwa na mifugo waliokufa wakati wa ukame kaskazini mwa nchi.
Ameongeza kuwa serikali pia itanunua mbuzi na kondoo 55,000 watakaotolewa kwa wakulima ili kuhakikisha kila familia inapokea usaidizi.
“Tumedhamiria kuhakikisha familia ambazo ziliwapoteza mifugo wao wakati wa ukame zinanufaika kutokana na mpango huo wa serikali,” alisema Rais Ruto.