Rais William Ruto amesema kuwa serikali yake imepiga hatua kubwa katika kuboresha viwango vya elimu hapa nchini, huku ikijizatiti kuhakikisha kuna walimu wa kutoka katika taasisi zote za masomo.
Kiongozi huyo wa taifa amesema tangu utawala wake ulipochukua hatamu za uongozi miaka mitatu iliyopita, imefanikiwa kuwaajiri walimu 76,000, idaid ambayo inalenga kuongeza hadi 100,000 kufikia Januari 2026.
Akizungumza Jumanne katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo ya Jamii Jijini Doha Qatar, Rais alisema hatua hiyo inalenga kutimiza pendekezo la Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu (UNESCO) la kuwa na mwalimu mmoja kati ya kila wanafunzi 25 kufikia mwaka 2027.
“Tunatambua kwamba elimu ni mojawepo wa nguzo za usawazishaji katika jamii. Ndio maana Kenya imekumbatia kikamilifu mfumo wa umilisi unaotoa fursa za uvumbuzi, ujuzi na elimu ya kiufundi,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto alidokeza kuwa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata soko tayari la ajira linalowiana na mahitaji ya kiviwanda na biashara, serikali yake imetekeleza jukumu muhimu la kupanua na kuongeza taasisi za kiufundi kote nchini
Alisema kupitia mpango wa kuboresha uchumi wa taifa hili kuanzia chini almaarufu Bottom Up, serikali imefanikiwa kukabiliana na changamoto kama vile umaskini, ukosefu wa usawa na ukosefu wa ajira miongoni mwa zingine.
					
			