Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir ameitaka serikali ya kitaifa kumakinika katika vita dhidi ya dawa za kulevya katika eneo la Pwani.
Akizungumza katika ukumbi wa Lohana,huko Majengo kaunti ndogo ya Mvita wakati wa kusambaza fedha za usaidizi wa masomo, Gavana huyo alisema serikali kuu ina kila inachohitaji kufanikisha vita hivyo.
“Sisi hatuna bunduki, hatuna ujasusi, hatuna lolote, msikae na mkatulaghai hapa kila siku. Mtwambie kwamba twawajua, tutawashika tuwafanya nini tutafanya nini, Washikeni!” alifoka Gavana Nassir.
Kiongozi huyo vile vile alisema kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya vina ncha mbili ambazo ni Kuzuia matumizi na ya pili kuzuia kuingizwa nchini kwa dawa hizo.
Alionya kwamba iwapo serikali itachelewa kuchukua hatua, atahimiwa wawakilishi wadi katika bunge la kaunti ya Mombasa waunde kikosi maalum cha kupambana na dawa za kulevya.
“Na kama hamuwezi nitawaambia hawa wabunge wa bunge la kaunti tutengeneze sheria tuwe na kikosi maalum cha kupigana na dawa za kulevya.” alisema kiongozi huyo.
Dawa za kulevya zimekuwa kero kubwa katika eneo la Pwani hasa mji wa Mombasa na Gavana Nassir anahisi wakati umewadia wa kuchukua hatua faafu.
Katika hafla hiyo Nassir alitangaza kusambazwa kwa shilingi milioni 200 karo ya wanafunzi wapatao elfu 40 chini ya mpango wa “Elimu Scheme”.
Walengwa ni wanafunzi wa shule za upili za kutwa kwenye wadi zote 30 za kaunti ndogo sita za Mombasa.