Baraza la Mawaziri limeidhinisha matumizi ya akaunti moja ya fedha, TSA itakayotumiwa na serikali kuu na zile za kaunti.
Hatua hiyo iliyoafikiwa wakati wa mkutano ulioongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatatu, inalenga kuboresha usimamizi wa fedha za umma.
Baraza la Mawaziri lilisitiza umuhimu wa kuwa na akaunti moja katika kurahisisha uwekaji wa fedha za serikali katika benki na kuimarisha uwazi katika usimamizi wa fedha hizo.
Mfumo huo mpya unatarajiwa kudhibiti matumizi ya fedha na kupunguza kuwepo kwa akaunti nyingi za serikali katika benki za kibiashara.
“Fedha za serikali zinawekwa katika benki za kibiashara na watu binafsi wanaendelea kupata riba. Hii inapaswa kukoma. Riba yote inayopatikana kwenye fedha za umma inapaswa kuwanufaisha Wakenya na wala si mtu mwingine yeyote,” alisema Rais Ruto.
Mfumo wa TSA utajumuisha Wizara ya Fedha, akaunti ndogo ya TSA na Hazina ya Mapato ya Kaunti.
Aidha katika hatua nyingine inayolenga kuhakikisha uwazi katika manunuzi ya serikali, Baraza la Mawaziri pia limeidhinisha utekelezaji wa mfumo wa kufanya manunuzi hayo kupitia kwa njia ya kielektroniki katika serikali kuu na zile za kaunti.
Mfumo huo unatarajiwa kuongeza usawa, uwazi, ushindani na kufanya manunuzi kwa gharama nafuu na yamkini kupunguza gharama kwa kati ya asilimia 10 hadi 15.
Hatua hii inaweza ikaifanya serikali kuokoa shilingi bilioni 90 kwa mwaka wakati ikifanya manunuzi.