Mafuriko yanayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali kufuatia mvua kubwa inayoenyesha nchini kwa sasa hayajafikia kiwango cha kutangazwa kuwa janga la kitaifa.
Kulingana na msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed, suala hilo lilijadiliwa wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatatu na kukubaliwa kuwa mafuriko hayo kwa sasa yamefikia kiwango hatari.
“Hatua ya kutangaza hali kuwa janga la kitaifa inatokana na data kutoka mashinani. Data ambayo imetathminiwa kutoka mashinani inaweka hali hii kufikia sasa kuwa katika hali ya hatari,” alisema Mohamed wakati akiwahutubia wanahabari katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatatu alasiri.
“Kuna kituo cha kitaifa cha kukabiliana na majanga kilichopo katika jumba la Nyayo kchini ya Wizara ya Usalama wa Kitaifa. Kinathmini data kutoka mashinani kila sekunde kubaini hali ilivyo. Kwa sasa, tupo katika kiwango cha hali hatari, ikiwa hali itazorota, basi serikali itakadiria hali hiyo na kutangaza mafuriko hayo kuwa janga la kitaifa.”
Kauli zake zikiwadia wakati viongozi kutoka kaunti za kaskazini mashariki mwa nchi wamekuwa wakiishinikiza serikali kuu kutangaza mafuriko hayo kuwa janga la kitaifa.