Serikali kutumia shilingi bilioni 2.3 kwa ujenzi wa vituo vya afya vya level 3

Tom Mathinji
2 Min Read
Serikali kujenga hospitali za level 3 kote nchini.

Serikali ya kitaifa itatumia kitita cha shilingi bilioni 2.3 katika kupandisha ngazi vituo vya afya hadi kiwango cha level 3, hayo ni kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha uboreshaji miundo msingi katika wizara ya afya Michael Thuita.

Thuita alisema kuwa mradi huo utakaotekelezwa kote nchini, utashuhudia kila kaunti kunufaika na shilingi milioni 50.

Aliyasema hayo katika kituo cha afya cha Urenga kilichoko wakilishi wadi ya Ugenya mashariki kaunti ya Siaya, katika hafla ya kupandisha kituo hicho cha afya kuwa cha level 3.

Kulingana na Thuita, kitakapokamilika, kituo hicho cha afya kitakuwa na kitengo cha kuwahudumia wagonjwa wa kulazwa, vifaa vya  X-ray pamoja na maabara, ili kuboresha utoaji huduma kwa wakazi wa eneo hilo.

“Huu ni mradi wa serikali ya kitaifa na mchakato huo wa kupandisha hadhi utachukua muda wa wiki 52,” alisema Thuita.

Alisema punde tu upandishaji ngazi wa kituo hicho cha afya utakapo kamilika, kituo hicho kitakabidhiwa serikali ya kaunti ya Siaya kwa usimamizi.

Aidha alitoa wito kwa serikali ya kaunti ya Siaya kuimarisha hali ya wafanyikazi katika kituo hicho cha afya, ili kuwaweza wakazi wa eneo hilo kufaidika na kituo hicho.

Mkurugenzi wa afya ya umma katika kaunti ya Siaya Kennedy Orwenjo, alipongeza serikali kuu kwa kufadhili mradi huo akisema utaimarisha pakubwa utoaji wa huduma za afya katika kaunti ndogo ya Ugenya.

Share This Article