Serikali ina mipango ya kutuma vikosi maalum kukabiliana na ukosefu wa usalama katika maeneo ya kaskazini mwa nchi na nyanda za juu za Pwani, zikiwemo kaunti za Tana River na Lamu.
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki amesema vikosi hivyo vitasaidia katika kuimarisha vita vya serikali dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab, wezi wa mifugo na wahalifu wengine ambao wamekuwa wakiwahangaisha wananchi wasiokuwa na hatia.
Aidha Kindiki ameelezea dhamira ya serikali ya kuwapa maafisa wa usalama silaha za kisasa na teknolojia ili kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na wahalifu.
“Ili kukabiliana ipasavyo na tishio la ugaidi na itikadi kali, serikali inavipeleka vikosi maalum kaskazini mwa nchi na nyanda za juu za Pwani zikiwemo kaunti za Tana River na Lamu ili kupambana vikali na kuwaangamiza wahalifu wanaowahangaisha wakazi wasiokuwa na hatia,” alisema Prof. Kindiki.
Aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa usalama ulioandaliwa katika eneo la Wayu, kaunti ndogo ya Galledyertu, kaunti ya Tana River akiandamana na Gavana wa kaunti hiyo Godhana Dhadho na Seneta Danson Mungatana miongoni mwa viongozi wengine.
Kindiki aliwahakikishia wananchi kwamba serikali imetenga fedha zaidi za kuwanunulia maafisa wa usalama vifaa na zana za kisasa, na kuongeza kuwa maafisa hao wamepewa ruhusa ya kikatiba kutumia silaha zao kulinda maisha na mali ya Wakenya.