Wizara ya Kilimo kutoa magunia milioni 12.5 ya mbolea kwa wakulima

Tom Mathinji
2 Min Read
Katibu katika wizara ya Kilimo Dkt. Paul Rono.

Serikali imetekeleza kikamilifu mpango wa usambazaji wa mbolea ya gharama nafuu kote nchini, kwa lengo la kuhakikisha taifa hili lina chakula cha kutosha.

Akizungumza leo Jumatatu katika kaunti ya Bungoma wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya kilimo kuhusu usalama wa chakula, katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Paul Rono, alisema katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024, serikali inalenga kutoa magunia milioni 12.5 ya kilo 50 ya mbolea kwa wakulima.

Kulingana na katibu huyo, ili kuhakikisha usalama wa chakula hapa nchini, wizara ya kilimo imewekeza katika mbinu bora na za kisasa za kilimo, ambazo ni pamoja na ukuzaji wa mimea inayostahimili ukame, uvunaji wa maji pamoja na usimamizi bora wa ardhi.

“Kama wadau katika sekta ya kilimo, tunatambua kwamba ili kuafikia usalama wa chakula na mageuzi katika sekta ya kilimo, ni kutokana na utumizi wa pembejeo bora za kilimo katika uzalishaji,” alisema Dkt. Rono.

Maonyesho ya kilimo katika kaunti ya Bungoma.

Rono alisema serikali pia inajizatiti kukabiliana na hasara itokanayo baada ya mavuno, kupitia kuwahamasisha wakulima na kutoa vifaa mwafaka kwa wakulima.

Maonyesho hayo ya kilimo ambayo yamefadhiliwa na wizara ya kilimo na ustawi wa mifugo, yanapigia debe utumizi wa mbinu bora za kilimo ili kuhakikisha taifa hili linajitosheleza kwa chakula.

Wengine waliohudhuria maonyesho hayo yaliyoandaliwa katika chuo kikuu cha Kibabii, ni pamoja na Gavana wa kaunti ya Bungoma Ken Lusaka na mwenzake wa Kakamega Fernandez Barasa.

Maonyesho hayo yatakamilika siku ya Ijumaa.

TAGGED:
Share This Article