Serikali kupitia Wizara ya Afya leo Alhamisi imezindua mpango unaolenga kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ya jamii 25,000 katika awamu ya kwanza kwa dhamira ya kuwaongezea ujuzi utakaoboresha utendakazi wao.
Mpango wa Afya ya Jamii iliyo Imara na Iliyowezeshwa Afrika, REACH ni ushirikiano wa pamoja kati ya serikali ya Kenya, Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Afrika cha Africa CDC, Shirika la Msalaba Mwekundu, IFRC na Prudence Foundation.
Wahudumu wote 107,831 waliosajiliwa na serikali kuu kwa ushirikiano na serikali za kaunti miezi michache iliyopita wamelengwa kupewa mafunzo chini ya mpango huo utakaotekelezwa kwa awamu.
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha ameusifia mpango huo akielezea nia ya serikali kuongeza upatikanaji wa huduma za afya vijijini na katika jamii kwa kuongeza idadi ya wahudumu wa afya na kuimarisha ujuzi wao kwa kushirikiana na washikadau wengine wa sekta ya afya.
“Mpango wa REACH ni mnara wetu wa matumaini na unawiana vyema na Ajenda ya Mabadiliko Kuanzia Chini hadi Juu (BETA) na Afya Nyumbani, na kuimarisha dhamira yetu ya upatikanaji wa afya kwa wote,” amesema Nakhumicha.
Kadhalika, mpango huo unaoungwa mkono na Umoja wa Afrika, AU unalenga kuimarisha utoaji huduma za afya ya msingi vijijini na unawalenga watu wasiojiweza katika jamii.
REACH pia inalenga kuongeza idadi ya wahudumu wa afya ya jamii hadi zaidi ya milioni 2 barani Afrika kufikia mwaka 2029.
Chini ya awamu ya kwanza, wahudumu wa afya zaidi ya 25,000 nchini watapewa mafunzo juu ya afya ya jamii na matumizi ya vifaa vya uhamasishaji wa afya ya jamii pamoja na mfumo wa kielektroniki wa afya ya jamii ili kuimarisha ufuatiliaji na ukadiriaji.