Serikali imetoa hakikisho kwamba itakuwa ikitoa kwa wakati pesa za matumizi ya shule za umma ili kuhakikisha zinatekeleza shughuli zake bila matatizo.
Akiongea wakati wa mkutano wa walimu wakuu wa shule za sekondari katika ukumbi wa shule ya Sheikh Zayed mjini Mombasa, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu aliwahakikishia walimu wakuu kwamba mikakati imewekwa ili kufanikisha utoaji wa fedha hizo kwa wakati.
Aidha alisema mgao wa ziada wa kifedha kwa wizara ya elimu katika bajeti ya kipindi cha fedha cha mwaka ujao utafanikisha utekelezaji wa masomo ya sekondari ya chini, JSS na utanufaisha takriban wanafunzi milioni 5 chini ya mpango wa lishe shuleni.
Machogu wakati huo huo aliwahimiza vijana kujiunga na kozi ya miezi minne katika vyuo vya kiufundi ili kuwawezesha kupata nafasi za ajira katika nchi za kigeni.
Aliwahimiza walimu kuendeleza masomo yao mitandaoni.
Walimu wakuu zaidi ya 900 kutoka shule za upili za serikali wanakongamana jijini Mombasa ili kujadili matumizi ya fedha na kutekelezwa kwa mtaala mpya wa CBC miongoni mwa masuala mengine yanayoathiri sekta ya elimu.