Serikali kutekeleza mabadiliko ya kupunguza ajali za barabarani

Kuanzia Julai, 2026, ukaguzi wa lazima wa magari utatekelezwa pamoja na uwekaji wa kamera za ulinzi katika miji mikubwa ili kurahisisha utekelezaji wa mabadiliko hayo.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesema kwamba serikali inatekeleza mabadiliko muhimu, yanayolenga kupunguza ajali za barabarani humu nchini.

Katika taarifa, kiongozi wa nchi alisema mabadiliko hayo yanajumuisha faini za papo hapo, kuanzishwa kwa mfumo wa kupunguzia madereva alama za ubora na kuratibiwa upya kwa makosa madogo ya trafiki kutoka kuwa jinai na kuwa makosa ya kiusimamizi.

“Kuanzia Julai 2026, ukaguzi wa lazima wa magari utatekelezwa pamoja na uwekaji wa kamera za ulinzi katika miji mikubwa ili kurahisisha utekelezaji wa mabadiliko hayo,” alisema kiongozi wa nchi.

Ruto pia alisema wanaangazia ubunifu wa kidijitali ili kupunguza ufisadi, kuanzisha utoaji wa vyeti kwa madereva wenye ujuzi wa kuendesha magari katika hatari na kuhalalisha vyama vya ushirika vya akiba na mikopo vya waendesha bodaboda.

Kulingana naye, kuafikia mabadiliko endelevu katika usalama barabarani kunahitaji uhusika wa serikali nzima na umma kwa jumla.

“Tunapotekeleza wajibu wetu, tunaomba Wakenya wote kutii sheria za trafiki na kuendelea kujali watumizi wenzao wa barabara.”

Aliyasema hayo alipopokea ripoti ya Baraza la Kitaifa la Utekelezaji Haki katika Ikulu ya Nairobi leo ambapo pia alisema usalama wa raia wa Kenya barabarani umepatiwa kipaumbele.

Kulingana na takwimu alizotoa kiongozi wa nchi, Kenya hunakili ajali zaidi ya elfu 4 za barabarani kila mwaka, huku vifo 5,009 vikiripotiwa mwaka jana pekee, ongezeko la vifo 261 ikilinganishwa na mwaka 2024.

Alifichua kwamba mfumo wa haki wa mashirika mbalimbali wa trafiki ulibuniwa na kujaribiwa msimu wa sherehe mwisho wa mwaka jana na mwanzo wa mwaka huu chini ya mfumo wa Baraza la Kitaifa la Utekelezaji wa Haki.

Mfumo huo uliofanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 10, ulihusisha mahakimu 36, maafisa 40 wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi na wenzao 121 wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani.

Share This Article