Katibu katika Wizara ya Elimu ya Juu Dr. Beatrice Inyangala amesema serikali ina mipango ya kufungua Chuo Kikuu cha Wazi cha Kenya kwa lengo kuu la kuwawezesha wanafunzi wanaofuzu kudahiliwa katika vyuo vikuu vya umma kujiunga na chuo hicho.
Dr. Inyangala aliyasema hayo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru wakati wa kongamano la kutathmini utafiti na hatua iliyopigwa kuelekea kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs kufikia mwaka 2030.
Aidha alisema serikali inadhamiria kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu vya umma wanaosomea kozi za uhandisi na teknolojia kutoka asilimia 20 hadi 60.
Kwa upande wake, Makamu Chansela wa Chuo Kikuu cha Meru Romanus Odhiambo alisema vyuo vikuu vinakabiliwa na changamoto kubwa kwani hakuna ufadhili wa kuwezesha utafiti mbalimbali katika elimu ya juu, kitu kinachofanya iwe vigumu kwa maprofessa kutekeleza utafiti wao.
Mwenyekiti wa Muungano wa Haki ya Tabia Nchi barani Afrika, PACJA Mithika Mzalendo alielezea changamoto inazokumbana nazo serikali katika kufikia maono ya mwaka 2030 ambayo yamejikita kwa SDGs.
Huku ikisalia miaka saba kabla ya kufikiwa kwa maono ya mwaka 2030, Mzalendo alisema janga la virusi vya korona halipaswi kuwa kisingizio lakini alitaja ukosefu wa ufadhili kuwa kikwazo kikuu kwa kufikiwa kwa maono ya mwaka 2030.