Waziri mwenye mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi, amesema serikali itaweka mikakati ya kuongeza idadi ya shule za umma za msingi na upili, ili kuwapunguzia mzigo wazazi ambao hawawezi mudu karo ya shule za kibinafsi.
Kulingana na Mudavadi, idadi ya shule za umma ni ya chini ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi inayoongezeka hapa nchini.
“Tunahitaji kutafuta njia za kuwekeza zaidi katika shule za umma kote nchini. Kulingana na takwimu, idadi ya shule za umma ni chache huku zikiwa na shinikizo za kuwachukua idadi kubwa ya wanafunzi ambayo haziwezi kumudu,”alisema Mudavadi.
Mudavadi aliyasema hayo Jumatatu asubuhi alipoongoza ufunguzi wa karatasi za mtihani wa darasa la nane KCPE na ule wa KPSEA katika shule ya msingi ya St Georges jijini Nairobi.
Akiwapongeza wadau wa sekta ya elimu waliohusika katika utayarishaji na usimamizi wa mitihani ya kitaifa ya mwaka 2023, Mudavadi alisema mitihani ya mwaka huu inapaswa kuwa na ubora wa hali ya juu zaidi.
“Nimefahamishwa kuhusu taratibu zilizofuatwa katika utayarishaji wa mitihani ya kitaifa ya mwaka huu, na ningependa wakenya kutambua kujitolea kwa hali ya juu na bidii za wadau katika sekta ya elimu kuhakikisha ufanisi wa zoezi hili,” aliongeza Mudavadi.
Jumla wa wanafunzi 1,202, 574 wanafanya mtihani wa tathmini wa gredi ya sita KPSEA na huku wanafunzi 1,415,315 wakifanya mtihani wa darasa la nane KCPE.