Serikali inapania kuongeza idadi ya vijana ambao husajiliwa katika taasisi ya huduma ya vijana kwa taifa, NYS kila mwaka hadi vijana elfu 20.
Akizungumza wakati akiongoza hafla ya 88 ya kufuzu kwa vijana hao huko NYS Gilgil kaunti ya Nakuru, Rais William Ruto aliahidi kwamba serikali itaongeza idadi hiyo kwa vijana elfu tano kila mwaka hadi itimie elfu 20.
“Nataka nitangaze hapa kwamba tutaongeza vijana ambao watakuja NYS,” alisema Rais Ruto akiongeza kwamba usajili unaofuata utatekelezwa katika kiwango cha kijiji ili kuhakikisha kila mmoja anapata fursa.
Kutokana na hilo, miundombinu ya taasisi ya NYS kote nchini itaboreshwa ili kutoa nafasi kwa vijana zaidi watakaosajiliwa. Rais aliagiza Wizara ya Nyumba kuhakikisha mabweni zaidi yanajengwa kwenye taasisi hiyo.
Shughuli kuu iliyotengewa vijana waliofuzu leo kulingana na Rais ni utunzaji wa mazingira nyanjani, chini ya mpango uitwao “Climate Works mtaani”.
Baada ya kuhudumia taifa kwa muda wa miaka minne ijayo, Rais alisema vijana waliofuzu leo watapata kozi mbalimbali ambazo zitawawezesha kujikimu kimaisha.
Alifafanua kwamba ameagiza Wizara ya Elimu kujumuisha vyuo vya mafunzo ya kiufundi vya NYS kwenye orodha ya vile ambavyo vitapatiwa vifaa ili kuhakikisha vijana wa NYS nao wanapata kozi mbalimbali.