Waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki leo alizuru shule ya upili ya wavulana Cheptulel ambayo iko katika eneo bunge la Sigor kaunti ya Pokot Magharibi kujionea hali halisi ya shule zilizotelekezwa kufuatia ukosefu wa usalama.
Kindiki amesema serikali itakarabati shule hizo na ndiyo sababu ameamua kuzizuru ili kufanikisha mipango ya ukarabati kuzitayarisha kwa ufunguzi wa shule Januari mwakani na kurejelewa kwa shughuli za masomo.
Kulingana naye, hilo linaambatana na sera ya serikali kwamba kila mtoto anastahili kupata elimu.
Shule ambazo zitafunguliwa tena chini ya mpango huo ni ile ya msingi ya Chesegon, shule ya msingi ya Cheptulel, sekondari ya wavulana ya Cheptulel, shule ya msingi ya Sapulmoi na ile ya chekechea ya Kisaa katika kaunti ndogo ya Pokot ya kati.
Nyingine ni shule ya msingi za Lonyangalem, Kour na Songok katika kaunti ndogo ya Pokot Kaskazini.
Waziri Kindiki alisema kwamba serikali itajazilia juhudi za kuhakikisha usalama katika mpaka wa kaunti za Baringo, Elgeyo Marakwet na Turkana kwa polisi wa akiba wapatao 205.
Polisi hao wa akiba wanaanza mafunzo kesho katika taasisi ya mafunzo kwa walimu ya Chesta eneo bunge la Sigor.
Haya yanajiri huku “Operation Maliza Uhalifu” ikiingia mwaka wa pili na wakenya wameonywa dhidi ya kuingiza ukabila, siasa au utambuzi wa aina nyingine katika masuala ya usalama.