Serikali ya kitaifa imejitolea kukamilisha miradi yote ya miundombinu iliyokwama katika eneo la Nyanza, kabla ya kuanzisha mipya katika hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza wakati wa kutoa vyakula vya misaada kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko katika shule ya upili ya Masara, eneo bunge la Muhoroni, Katibu waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali Eliud Owalo alithibitisha kuwa serikali imeweka masharti ya kusaidia ukamilishaji wa miradi muhimu ya maendeleo katika eneo hilo.
Miongoni mwa miradi iliyoratibiwa ni pamoja na uwekaji lami barabara ya Mamboleo-Miwani-Chemelil-Muhoroni-Kipsitet, ya umbali kilomita 63, ambayo ilianzishwa mwaka 2022 lakini ilikabiliwa na changamoto za ufadhili.
Waziri Owalo amefichua kuwa Ujenzi wa Barabara ya Kisiwa cha Mfangano kaunti ya Homa Bay umekamilika baada ya kuzinduliwa na Rais William Ruto mwezi uliopita.
Mbali na miradi ya miundombinu, serikali pia inalenga kufufua sekta ya sukari katika kanda hiyo.
Licha ya kukabiliwa na changamoto, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kisheria, Owalo alitangaza kuwa serikali imeanzisha malipo ya malimbikizo kwa wakulima na wafanyakazi wa miwa katika kampuni tano za sukari zinazomilikiwa na serikali.
Mipango ya kukodisha kampuni za sukari za Nyanza Kusini, Nzoia, Miwani Sugar, Muhoroni na Chemelil kwa wawekezaji wa kibinafsi inalenga kufufua shughuli na kuchochea shughuli za kiuchumi katika sekta ya sukari.
Owalo pia alifichua kuwa mipango ya kuanzishwa kwa vituo vya kidijitali katika wadi zote nchini, kwa ushirikiano na Hazina ya ustawishaji maeneo bunge (NG-CDF).
Vituo hivyo vitatoa mafunzo ya kidijitali na fursa za ajira, hasa kwa waliomaliza kidato cha 4 na wahitimu, ili kushughulikia ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.