Serikali inapanga kujenga mabwawa zaidi ya 100 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kama njia ya kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa kote nchini.
Waziri wa maji na unyunyiziaji mashamba maji Zachary Njeru ameashiria kurejelewa kwa mradi uliokwama wa bwawa la Itare katika kaunti ya Nakuru, akisema tayari pesa za mradi huo zimetengwa kwenye bajeti.
Kilingana na waziri Njeru, watu zaidi ya laki 6 wa kaunti za Baringo na Nakuru hivi karibuni watakuwa na maji safi na salama kwenye boma zao, kufuatia kukamilika kwa mradi wa bwawa la Chemususu.
Akizungumza huko Nakuru alipozindua usambazaji wa chakula cha msaada kilichotolewa na jamii ya waisilamu kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhan, Njeru alisema kando na kutoa maji kwa wakazi, mabwawa ya Itare na Chemususu yatatoa nafasi za ajira.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuangazia kilimo cha kunyunyizia mashamba maji kutokana na tabianchi isiyotegemewa ambayo imesababisha kilimo cha kutegemea mvua kuwa hatari.
Njeru alisema serikali ya kitaifa inajibidiisha kuongeza eneo la kilimo cha kunyunyizia mashamba maji hadi ekari milioni tatu kufikia mwaka 2030.