Spika wa bunge la Taifa Moses Wetangula amesema kwamba serikali inapanga kujenga barabara yenye safu mbili kila upande kama njia ya kusuluhisha msongamano wa magari ambao hushuhudiwa kila mara kutoka Eldoret kuelekea mji wa mpakani wa Malaba.
Alikuwa akizungumza jana Jumapili kwenye hafla ya ibada na mchango katika kanisa katoliki la Our Lady of Lourdes huko Malaba eneo la Teso Kaskazini kaunti ya Busia.
Wetangula ambaye aliongoza wabunge wapatao 12 wa eneo la magharibi mwa nchi kuchangia kanisa hilo alisema barabara hiyo itakapojengwa itakuwa suluhisho la kudumu kwa matatizo yanayokumba waendeshaji magari ya mizigo na kupunguza hasara ambayo hutokana na bidhaa kuharibikia njiani.
Alisema hata ingawa serikali inakumbwa na matatizo ya kifedha, atahakikisha miradi kama huo wa barabara na wa bandari ya nchi kavu inapatiwa kipaumbele kwani ni muhimu.
“Kituo cha mpaka cha Malaba kinahudumia nchi kama Uganda, Congo na Rwanda na kina uwezo mkubwa kiuchumi.” alisema Wetangula akiongeza kwamba kwa sababu hiyo, bandari ya nchi kavu itachochea biashara na uwekezaji.
Spika huyo alifichua pia mipango ya serikali kuendeleza reli ya kisasa SGR hadi Malaba hatua aliyosema inadhihirisha kujitolea kwa serikali katika uunganishwaji wa kanda.
Kuhusu umoja kati ya watu wa jamii ya Luhya, Wetangula aliambatanisha migawanyiko inayoshuhudiwa na viongozi wao.