Katika juhudi za kuimarisha kilimo cha majani chai hapa nchini, Serikali imesisitiza kujitolea kwake kupiga jeki kilimo hicho, kupitia majadiliano na ushirikiano.
Akizungumza alipozuru kiwanda cha majani chai cha Kapset siku ya Ijumaa, katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, alipongeza juhudi na uvumbuzi zinazotekelezwa na kiwanda hicho, ambazo zimechangia pakubwa kwa ukuaji na ufanisi wa shughuli za uzalishaji majani chai.
Wakati wa ziara hiyo, katibu huyo aliahidi kufanyia mageuzi operesheni kwa kutathmini mchakato wa uzalishaji wa kiwanda hicho, vifaa na ufanisi wake kuhakikisha vinaafikia viwango vinavyohitajika vya kiviwanda.
Wakati huo huo Dkt. Ronoh alidokeza kuwa wizara yake itashughulikia changamoto zinazowakumba wakulima kwa kupigia kurunzi maswala ya kipekee yanayokumba kiwanda hicho, kama vile matatizo ya usambazaji, upungufu wa nguvukazi na uhaba wa fedha.
Aidha alisema serikali itatatua maswala yaliyoibuliwa na wakulima wa majani chai wa eneo hilo, akiahidi kuimarisha uungwaji mkono huku akielezea matumaini kuhusu maendeleo katika siku za usoni.
“Hatua hiyo huenda ikahusisha mikakati ya serikali ya kuboresha sekta ya majani chai sawia na kuimarisha maisha ya wakulima wa majani chai,” alisema Dkt. Ronoh.
Ziara hiyo katika kiwanda cha majani chai cha Kapset, baada ya kuzuru kile cha Momul Ijumaa subuhi, ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha viwango bora vya majani chai katika viwanda pamoja na kushinikiza kuimarika kwa marupurupu na bei kwa manufaa ya wakulima.
Vile vile ziara hiyo ililenga kuimarisha mawasiliano kati ya serikali na viwanda vya majani cha, kuhakikisha viwanda hivyo pamoja na wakulima wanapokea msaada na rasilimali zinazohitajika.
Kulingana na katibu huyo, uimarishaji wa viwango vya uzalishaji majani chai ni muhimu na unapaswa kupewa kipaumbele na viwanda vya majani chai.
Katika ziara hiyo, katibu huyo aliandamana na viongozi wa kisiasa wa eneo hilo na naibu mkurugenzi wa kampuni za majani chai za Kapset na Rorok, Ian Kipsang.