Serikali kufanyia mabadiliko kalenda ya shule kufidia muda uliopotea

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu azuru shule kadhaa kaunti ya Nairobi.

Waziri wa elimu, Ezekiel Machogu, ametangaza kwamba serikali itaongeza muda wa muhula wa pili ili kufidia muda uliopotea baada ya kuahirishwa kufunguliwa kwa shule kwa wiki mbili kutokana na mafuriko.

Machogu ambaye alizungumza alipokuwa akizuru shule kadhaa jijini Nairobi kutathmini uharibifu uliosababishwa na mafuriko na utayari wa shule kufunguliwa, alisema muhula wa pili utaongezwa kwa muda ambao bado haujaamuliwa ili kuwezesha shule kukamilisha silabasi kabla ya mitihani ya kitaifa ya mwaka huu mwezi Novemba.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mitihani ya Kitaifa ya Shule za Upili – KSCE na Shule ya Msingi – KPSEA haitaahirishwa.

Waziri huyo aliondoa hofu ya utovu wa usalama kwa wanafunzi wakati shule zitafunguliwa, akisema serikali imetathmini hali hiyo na kubaini kuwa inaweza kudhibitiwa.

Kulingana na Machogu, baadhi ya shule katika kaunti saba miongoni mwao Tana River, Homa Bay na Kisumu, huenda hazitafunguliwa tena Jumatatu, na kwa hivyo, wizara itatafuta njia mbadala za kuhakikisha wanafunzi warejelea masomo kama vile kuhamishwa kwa wanafunzi hadi vituo vilivyo salama.

Share This Article