Serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na serikali za kaunti imeanzisha ujenzi wa maeneo ya viwanda katika kila kaunti.
Katika mkutano na wadau siku ya Jumatatu afisni mwake mtaani Karen, naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, alisema ujenzi wa awamu ya kwanza ya maeneo ya viwanda 19 umepiga hatua kubwa, huku awamu ya pili ya ujenzi wa maeneo 16 ukiwa kwenye mpango.
“Ujenzi wa awamu ya kwanza ya maeneo 19 ya viwanda umepiga hatua huku ujenzi wa awamu ya pili ukiendelea,” alisema Profesa Kindiki.
Aidha, kulingana na naibu huyo wa Rais, alisema ipo ya haja ya kuwa na mikakati ya uzalishaji na uongezaji bidhaa thamani pamoja na uhamasishaji wa wadau wote wakiwemo wawekezaji.
Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ahmed Abdullahi, mawaziri husika, makatibu katika wizara na maafisa wa ngazi za juu katika serikali kuu na zile za kaunti.