Rais William Ruto amesema serikali itanunua ardhi isiyotumiwa na kuwapa maskwota ardhi hiyo katika eneo la pwani.
Waliopewa jukumu kuhakikisha hatua hiyo inafanikiwa ni pamoja na spika wa bunge la Seneti Amason Kingi, mawaziri Alice Wahome wa ardhi, mwenzake wa uchimbaji madini Hassan Joho, na yule wa Michezo Salim Mvurya.
Kulingana na agizo la Rais, viongozi hao wanatarajiwa kuwatambua wamikili halisi wasiotumia ardhi yao kwa vyovyote, ili waweze kulipwa na serikali kwa ardhi hiyo kisha ipatiwe maskwota.a
Kiongozi wa taifa alisema hatua hiyo ni muhimu katika juhudi za kutataua dhulma za jadi zilizowakumba wakazi wa eneo la pwani wengi wao wakibaki bila stakabadhi za kumiliki ardhi.
Rais Ruto aliyasema hayo wakati wa hafla ya mazishi ya babake spika wa bunge la seneti Mzee Kingi Mwaruwa Mkweha, katika sehemu ya Kamale, Magarini eneo bunge la Kilifi.
Rais aliwahakikishia maskwota katika kaunti hiyo kwamba serikali iko kwenye utaratibu wa kutatua changamoto za umiliki wa ardhi katika sehemu hiyo na kuwahakikishia watapokea hatimiliki za ardhi baadaye mwaka huu.
Rais anatarajiwa kuandaa ziara ya siku tano ya kikazi wiki ijayo katika eneo la Pwani ambako atazuru kaunti za Lamu, Tana River, Kwale, Kilifi, Mombasa na Taita-Taveta.