Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kiprono Rono amesema sekta ndogo ya Majani Chai, ni mojawepo wa nguzo za kilimo hapa nchini, ambayo inasaidia familia nyingi kujikimu, na hivyo kuifanya serikali kujizatiti kuimarisha sekta hiyo.
Dkt. Ronoh aliyasema hayo alipofanya ziara ya ukaguzi katika kiwanda cha Majani Chai cha Githongo kaunti ya Meru.
Aidha katika ziara hiyo, katibu huyo alishauriana na wakulima, huku akitathmini hali ya utoshelevu wa chakula katika eneo hilo.
Dkt. Ronoh pia alizindua zoezi la usambazaji mbegu za upanzi, tayari kwa msimu wa upanzi wa mwezi Novemba hadi Januari wakati wa kipindi cha mvua.
“Serikali iko makini kutekeleza mpango wa kiuchumi kutoka chini almaarufu BETA, ambayo inalenga kuzipa pengo la kijamii na kiuchumi kupitia upatikanaji wa rasilimali na mazingira bora kwa wakenya wote,” alisema Dkt. Rono.
Katika ziara hiyo katibu huyo alikuwa ameandamana na wabunge kadhaa wa eneo hilo, pamoja na mwenyekiti wa shirika la kukadiria ubora wa mimea Joseph M’eruaki,miongoni mwa wengine.