Serikali imesambaza magunia milioni 16 ya mbolea ya bei nafuu

Tom Mathinji
1 Min Read
Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh.

Serikali imesambaza magunia milioni 16 ya kilo 50 ya mbolea ya gharama nafuu, tangu ilipochukua usukani miaka miwili iliyopita.

Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, amesema hatua hiyo imefanikisha ukuzaji wa chakula hapa nchini na kuhakikisha taifa hili lina utoshelevu wa chakula.

kulingana na Dkt. Ronoh, mbolea hiyo ya gharama nafuu ni ya ubora wa kiwango cha hali ya juu, na ni maalum katika maeneo tofauti .

Aidha katibu huyo alisema awali wakulima walilazimika kusafiri mwendo mrefu kuchukua mbolea hiyo, lakini sasa serikali imehakikisha mbolea hiyo inapatikana karibu na wakulima, hatua iliyosababisha kuimarika kwa ukuzaji wa chakula hapa nchini.

Ili kuhakikisha ufanisi katika usambazaji wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima, Dkt. Ronoh alisema wizara ya kilimo ilibuni kundi la maafisa wa asasi mbalimbali, kuchunguza kila hatua ya usambazaji huo.

Alisema kati ya magunia milioni 16 ya mbolea hiyo, ni magunia 5,000 tu yaliyopatikana kuwa na kasoro.

“Wakati wa usambazaji, tuligundua kasoro katika aina moja ya mbolea, na tulisitisha usambazaji wake baada ya takriban magunia 5,000 kusambazwa,” alisema Dkt. Ronoh.

Alidokeza kuwa serikali imewasajili wakulima milioni 6.4, ikinakili jina, sehemu waliko, ukubwa wa shamba na aina ya mimea wanayokuza.

Share This Article