Rais William Ruto amesema atatumia kikamilifu mamlaka yake ya kikatiba kulinda rasilimali za umma.
Aliwahakikishia Wakenya kwamba Serikali itatumia ushuru kwa busara katika kutekeleza mipango ya maendeleo.
“Kama ushuru wenu umefujwa, niwajibisheni,” alisema.
Alizungumza hayo siku ya Alhamisi wakati wa ibada katika kanisa la ACK St James Cathedral katika Kaunti ya Kiambu, ambapo pia aliweka jiwe la msingi kwa kanisa hilo na baadaye kuhutubia wakazi wa Mji wa Kiambu.
Rais alisema hataruhusu wanaomkejeli kukwamisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Serikali.
“Tuna fursa ya kihistoria ya kubadilisha hatima ya taifa letu,” aliongeza.
Alibainisha kuwa Serikali ina nia ya kubuni fursa kwa vijana katika mpango wa makazi na uchumi wa kidijitali.
Rais Ruto alitoa wito kwa wakulima ambao bado hawajajisajili kufanya hivyo ili kuiwezesha Serikali kutoa usaidizi unaolengwa.
Alisema lengo ni kuongeza uzalishaji wa chakula, kupunguza gharama ya maisha na kuongeza kipato cha wakulima.
“Bei ya bidhaa za chakula inashuka kwa sababu tulikuwa na mtego mkubwa wa madeni.”
Rais alisema Serikali imepunguza kukopa ili kuinusuru nchi isiingie kwenye mtego wa madeni.
“Hatuwezi kuendelea kukuza uchumi wetu kwa madeni, tutakuza uchumi wetu kwa kutumia rasilimali zetu,” alisema kiongozi wa taifa.