Waziri wa Elimu Julius Ogamba anasema serikali kufikia sasa imejenga madarasa 14,500 ya kutumiwa na wanafunzi wa Gredi ya 9.
Ameongeza kuwa serikali inakusudia kufikisha 16,000 mwishoni mwa mwezi huu idadi ya madarasa yaliyojengwa ya kutumiwa na wanafunzi hao.
“Hii imewezeshwa na usambazaji wa shilingi bilioni 11 kwa shule kote nchini kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 11,000 ya Gredi ya 9,” amesema Ogamba.
“Shilingi bilioni 6.8 zilitengewa NG-CDF (zinazojumuisha shilingi bilioni 3.4 kutoka kwa Wizara ya Elimu na shilingi bilioni 3.4 kutoka kwa NG-CDF) kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 6,800.”
Waziri amesema madarasa mengine 7,290 yatajengwa ili kukidhi ongezeko la wanafunzi ambalo limeshuhudiwa nchini.
Serikali imekabiliwa na shutuma kwa kutojiandaa vyema kwa wanafunzi wa Gredi ya 9 huku shule nyingi zikisemekana kutokuwa na madarasa yanayohitajika ya kutumiwa na wanafunzi hao.