Naibu msemaji wa serikali Mwanaisha Chidzuga, amesema serikali haitawafidia waliojenga nyumba katika mikondo ya maji.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio , Chidzuga alisema uchunguzi umebaini kuwa watu hao walibadili mikondo ya maji na mito na kujenga makazi hapo.
Alisema kuwa baada ya mafuriko kusomba nyumba zao, sasa wanataka fidia kutoka kwa serikali.
“Kama unajua umebadili mkondo wa mto, sogea tu. Hatutakupa fidia ya kununua ardhi mahali pengine,” alisema Chidzuga.
Naibu msemaji huyo alisema serikali ya Rais William Ruto imetenga fedha za kutoa fidia kwa waathiriwa halali wa mafuriko.
“Kuna fidia ambapo tumetenga shilingi bilioni 39 kukabiliana na mafuriko,” alieleza.
Chidzuga aliongeza kuwa wale waliolaghaiwa wakati wa kupewa hati miliki ya ardhi watapata fidia, akiongeza kuwa watapewa ardhi mbadala au raslimali nyingine kwa minajili ya makazi mapya.