Serikali haina nia ya kufutilia mbali elimu bila malipo, abainisha Katibu Bitok

Martin Mwanje
3 Min Read
Prof. Julius Bitok - Katibu wa Idara ya Elimu ya Msingi

Katibu wa Idara ya Elimu ya Msingi Prof. Julius Bitok sasa anasema serikali haina nia ya kufutilia mbali elimu bila malipo. 

Prof. Bitok anasema Wizara ya Elimu italitaka bunge kuongeza mgao wa fedha kwa wizara hiyo ili kuiwezesha kufadhili elimu katika shule za umma.

Katibu huyo ameyasema hayo leo Ijumaa wakati wa siku ya kutoa tuzo katika shule ya upili ya wasichana ya St. Thomas katika kaunti ya Kilifi.

Hakikisho lake linakuja wakati ambapo serikali imeshutumiwa vikali kutokana na tangazo kuwa haitafadhili kikamilifu elimu ya msingi bila malipo kutokana na uhaba wa fedha.

Akizungumza jana Alhamisi alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Taifa juu ya Elimu kujibu masuali kuhusiana na sekta ya elimu nchini, Waziri wa Fedha John Mbadi aliwaambia wanachama wa kamati kwamba serikali haina fedha za kutosha kuendelea kufadhili kikamilifu mpango wa elimu ya msingi bila malipo.

Mpango huo ulianzishwa na utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hii, Hayati Mwai Kibaki.

Kauli ambazo ziliibua shutuma kutoka kila pembe.

Chama cha KUDHEIHA kimeelezea hofu kuwa hatua hiyo, ikiwa itachukuliwa,  itawanyima wanafunzi wengi hasa kutoka familia maskini haki ya kupata elimu bora.

Katibu Mkuu wa chama hicho Albert Njeru ametoa wito kwa serikali kubatilisha hatua hiyo anayosema itakuwa na madhara makubwa kwa sekta ya elimu nchini.

Kauli sawia zimetolewa na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

“Mambo ya Free Basic Education, hatumwomba mtu yeyote. Tunasema ni lazima mpango huo uendelee,” alisema Nyoro ambaye wakati mmoja alikuwa mwenyekti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Taifa.

“Hatutakubali yeyote kufanya mchezo na suala la elimu ya msingi bila malipo. Chumi hujengwa na watu, kazi ya elimu ni kuongeza thamani kwa watu, kwa wafanyakazi katika mantiki ya kiuchumi. Elimu huongeza thamani kwa wafanyakazi ambao ni watu, na uchumi wa Kenya unaweza kukua tu ikiwa elimu itapatikana kwa wote, ni elimu bora na kila mtu ako na fursa ya kuipata,” aliongeza mbunge huyo aliyezungumza katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA.

Waziri wa zamani wa Elimu Dkt. Fred Matiang’i, akigusia suala hilo alipendekeza kusitishwa kwa baadhi ya mipango inayotekelezwa na serikali kama ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ili fedha zinazotumiwa kwenye mipango hiyo zitumiwe kufadhili mpango wa elimu bila malipo nchini.

Matiang’i ambaye ametangaza azima yake ya kuwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2027 ameahidi kurejesha ufadhili kamili wa mpango wa elimu bila malipo ikiwa atapewa fursa ya kuiongoza nchi.

 

 

Share This Article