Serbia yalaani hatua ya Kenya ya kutambua Kosovo

Rais William Ruto jana alifanya mkutano na mjumbe maalum wa Rais wa Kosovo Vjosa Osmani aitwaye Behgjet Pacoli katika ikulu ya Nairobi.

KBC Digital
2 Min Read

Serikali ya Serbia kupitia kwa Wizara ya Mambo ya Nje imelaani vikali hatua ya serikali ya Kenya ya kutambua uhuru wa eneo la Kosovo.

Katika taarifa kwenye akaunti rasmi ya wizara hiyo kwenye mtandao wa X, Serbia imesema kwamba hatua ya Kenya ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na azimio nambari 1244 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Azimio hilo linathamini kwa kauli moja uhuru na uadilifu wa mipaka ya taifa la Serbia.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Kenya kutambua Kosovo kama taifa kwa kile ilichokitaja kuwa amani na usalama wa kimataifa, uadilifu wa mipaka na kuendeleza uimarishaji wa uhusiano na nchi za eneo la Balkans.

Katika taarifa kwenye kitandazi cha X,  akaunti ya Idara  ya Masuala ya Kigeni ya Kenya, idara hiyo ilielezea kwamba tamko la uhuru wa Kosovo la Februari 17, 2008 liliungwa mkono na mahakama ya kimataifa ya haki mwaka 2010.

Rais William Ruto jana alifanya mkutano na mjumbe maalum wa Rais wa Kosovo Vjosa Osmani aitwaye Behgjet Pacoli katika Ikulu ya Nairobi, na picha ya pamoja ya Rais Ruto, Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi na wajumbe wa Kosovo imechapishwa huko.

Serbia inalalamika kwamba Kenya imechukua hatua hii wakati nchi hiyo inaadhimisha miaka 80 tangu kupitishwa kwa katiba ya Umoja wa Mataifa, UN ambayo inahisi Kenya imekiuka kwa kutambua Kosovo.

“Uamuzi huu unadhoofisha juhudi za mazungumzo, uthabiti wa kanda na heshima kwa mfumo wa kimataifa wa kisheria,” ilisema Wizara ya Mambo ya Nje ya Serbia katika taarifa.

Serbia inasema hatua ya kurejelea ushauri wa mwaka 2010 wa mahakama ya kimataifa ya haki haina msingi wowote na kwamba inatoa mfano mbaya kwa uhusiano wa miongo kadhaa kati ya Kenya na Serbia.

Taifa la Serbia sasa linatishia kuchukua hatua zote za kidiplomasia na kisiasa kujibu hatua iliyochukuliwa na Kenya.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *