Seneta wa Nakuru Tabitha Karanja mashakani

Martin Mwanje
2 Min Read

Mahakama leo Jumatano imetoa kibali cha kukamatwa kwa Seneta wa kaunti ya Nakuru Tabitha Karanja kwa kukosa kufika mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi ya kukwepa kulipa kodi ya shilingi bilioni 14. 

Mwezi Aprili mwaka huu, Karanja ambaye wakati huo alikuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Keroche Breweries Limited alishtakiwa upya katika kesi hiyo.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba kuifanyia mabadiliko hati ya mashtaka ya kesi hiyo.

Mawakili wa kampuni ya Keroche waliiambia mahakama kwamba wanataka kesi kusuluhishwa nje ya mahakama.

Hata hivyo, afisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini, KRA Irene Muthee aliiambia mahakama kuwa hapakuwa na makubaliano ya kusuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama kwa sababu kampuni ya Keroche itatakiwa kumtaarifu kamishna wa mamlaka hiyo kwa maandishi chini ya Sheria ya Utaratibu wa Kodi.

Kutokana na hilo, mahakama iliipa kampuni ya Keroche siku 45 kuanza mchakato wa kusuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama na KRA, na hilo lisipofanyika, kesi hiyo itasikilizwa kikamilifu.

“Ni dhahiri upande wa utetezi haukuwa tayari. Naupatia siku 45 kuanzisha mchakato mbadala wa kusuluhisha mzozo huo na hilo lisipofanyika, hakuna kucheleweshwa kwa aina yoyote au kuahirishwa kwa kesi kutakubaliwa. Mahakama daima iko tayari,” alisema Hakimu Mkuu Mkazi wa Milimani Esther Kimilu.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *