Seneta wa Nakuru atoa wito wa kutimuliwa kwa Gavana Susan kihika

Tom Mathinji
2 Min Read
Seneta wa Nakuru Tabitha Karanja.

Seneta wa kaunti ya Nakuru Tabitha Karanja ametoa wito wa kung’atuliwa mamlakani kwa gavana wa kaunti hiyo Susan Kihika, kutokana na mzozo unaotatiza utoaji wa huduma katika hospitali ya War Memorial.

Kulingana na Tabitha hatua ya serikali ya kaunti hiyo ya kuvamia hospitali hiyo na kuwaacha wagonjwa bila huduma za matibabu ambapo mgonjwa mmoja alifariki ni sababu mwafaka ya kumwondoa madakarani gavana huyo.

Haya yanajiri saa chache baada ya mgonjwa aliyekuwa akipokea matibabu katika hospitali hiyo kufariki jana asubuhi huku serikali ya kaunti hiyo ikishtumiwa kwa kukiuka agizo la mahakama.

Seneta Karanja alimlaumu Kihika kwa kile alichokitaja kuwa kutokuwa na utu huku familia ambazo mpendwa wao alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo zikiendelea kuteseka.

Akiongea na wanahabari mjini Naivasha, Karanja alisema ukodishwaji wa ardhi uliofanywa na hospitali hiyo ni wa halali na kwamba kuna baadhi ya watu wanaotaka kumiliki ardhi hiyo akisema wakati umewadia kwa wawakilishi wadi kuchukua hatua kwani kuna ushahidi wa kutosha kumng’atua mamlakani gavana huyo.

Huku akifariji familia zilizompoteza mpendwa wao, Tabitha alitoa wito kwa wizara ya afya kuingilia kati, ili kuhakikisha maisha zaidi hayapotei kutokana na mzozo huo.

Huku akiwa ameandamana na viongozi wa eneo hilo, Seneta huyo alidokeza kuwa sekta ya afya ya Nakuru ambayo hapo awali ilikuwa ikimezewa mate na maeneo jirani, sasa imesambaratika.

Share This Article