Seneta Osotsi avamiwa jijini Kisumu

Kulingana na Gavana Orengo, Osotsi alikuwa mkahawani akipata kahawa na rafiki alipovamiwa ghafla na wahuni.

Marion Bosire
1 Min Read

Seneta wa kaunti ya Vihiga Godfrey Osotsi alivamiwa na kuumizwa na watu wasiojulikana akiwa mjini Kisumu, wakati alikuwa amekwenda kinyozi.

Mwenzake wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna alithibitisha kisa hicho kupitia chapisho kwenye akaunti yake ya mtandao wa X ambapo aliongeza kusema kwamba alikuwa asafirishwe kwa ndege hadi Nairobi kwa ajili ya matibabu.

“Nimezungumza na wahudumu wa Seneta Osotsi na kuthibitisha kwamba kweli alivamiwa vibaya na kuumizwa huko Kisumu mapema leo, alipokwenda kinyozi,” aliandika Sifuna huku akilaani vikali kisa hicho na kutaka polisi kukichunguza.

Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo ambaye alimzuru Osotsi hospitalini Agha Khan Kisumu alikopelekwa, alielezea kwamba baada ya kunyolewa, Osotsi aliingia kwenye jengo la Acacia ambapo alikuwa anapata kahawa na rafiki.

Anasema vijana wadogo waliokuwa wamejihami waliingia kwenye mkahawa huo ghafla na kumvamia Seneta Osotsi na anasema ameumizwa vibaya mno.

Orengo ameomba picha za kamera za ulinzi kutoka kwa usimamizi wa mkahawa wa Java akisisitiza kwamba kitendo hicho sio cha vurugu za kawaida tu.

Baadaye akizungumza na wanahabari, Orengo alithibitisha kwamba alikuwa ameongoza mpango mzima wa Osotsi kuondolewa hospitalini Kisumu hadi uwanja wa ndege kwa ajili ya kuletwa Nairobi kwa matibabu.

Share This Article