Seneta mteule Gloria Orwoba amepigwa marufuku kukanyaga katika majengo ya bunge kwa muda wa miezi sita kwa kutoa madai ya uwongo dhidi ya Maseneta wenzake.
Orwoba anajulikana sana kwa kutetea haki za watoto wasichana kupewa visodo ili kuhakikisha safari yao ya masomo haitatiziki.
Bunge la Seneti jana Jumatano, kwa kauli moja lilipitisha hoja ya kumfungia nje Seneta huyo kwa kipindi cha miezi sita.
Yamkini Orwoba alitoa madai ya ufisadi na dhuluma za kunyanyaswa kimapenzi dhidi ya Maseneta wenzake, madai aliyoshindwa kuthibitisha na pia akadinda kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya bunge hilo ili kujitetea.
Hata hivyo, kupitia kwa njia ya video, Seneta huyo mteule amekana kuwahi kuitwa mara mbili kujitetea mbele ya kamati ya nidhamu kabla ya hukumu ya Jumatano.
Seneta huyo hatalipwa marupurupu ya vikao wakati wa marufuku hiyo.