Sekta ya benki yatakiwa kutumia teknolojia kutatua changamoto zilizopo

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto.

Rais William ametoa changamoto kwa sekta ya benki hapa nchini, kutumia teknolojia, ili kutoa bidhaa za kifedha zitakazotatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wadogo wadogo na wale wa kadri.

Akizungumza leo Jumatano katika jumba la mikutano ya kimataifa la Kenyatta KICC, kiongozi huyo wa taifa alisema serikali itaendelea kubuni mazingira bora ya kufanya biashara, ili kuimarisha ukuaji wa biashara hapa nchini.

“Hatua hii itabuni nafasi za ajira, kuinua maisha ya jamii nyingi na kupiga jeki ajenda ya kuimarisha uchumi wa taifa hili,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi huyo wa taifa wakati huo huo, alipongeza sekta hiyo ya benki kwa kujitolea kuongeza maradufu mikopo yao kwa biashara ndodo ndogo na za kadri.

Chama cha wana benki hapa nchini, kiliahidi kutoa shillingi billioni 450 kuinua biashara ndogo ndogo na za kadri kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka ujao.

Rais aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa sekta ya benki kuunga mkono biashara ndogo ndogo na za kadri na kutolewa kwa ripoti ya ushuru kutoka sekta ya benki ya mwaka 2023.

Vile vile alitoa wito wa juhudi za pamoja kati ya Benki na sekta ya umma, ili kuongeza msaada wa kifedha kwa sekta ya utayarishaji bidhaa kwa minajili ya  kuimarisha uwekezaji na ukuaji.

Share This Article