Sean Kingston aachiliwa

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Kisean Paul Anderson maarufu kama Sean Kingston ameachiliwa kutoka jela baada ya kulipa dhamana ya dola laki moja.

Kingston alikamatwa kuhusiana na kesi ambapo anadaiwa kulaghai wafanyabiashara kadhaa. Alikamatwa huko California Mei 23, 2024 ambako alikuwa amekwenda kutumbuiza.

Alihamishiwa jimbo la Florida Jumapili iliyopita baada ya kukubali kuhamishwa na alipolipa dhamana akaachiliwa Jumatano Juni 5, 2024.

Alichapisha picha kwenye akaunti yake ya Instagram ambazo zinamwonyesha akiwa kwenye makazi yake ambapo anapokea wageni akiwemo mamake na kusema kwamba alijihisi vyema kuwa nyumbani.

Mamake Kingston kwa jina Janice Turner naye alikamatwa siku ambayo Kingston alikamatwa kwa madai sawia ya kuendeleza mchakato wa ulaghai na wizi.

Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, wawili hao wanadaiwa kuiba sigha za thamani ya juu, pesa, gari aina ya Cadillac Escalade na samani za thamani ya juu.

Kingston tayari alikuwa anatumikia kifungo cha nje cha miaka miwili kufuatia makosa ya kupatikana na bidhaa zilizoibwa.

Mamake pia sio mgeni kwa uhalifu, aliwahi kukamatwa mwaka 2006 na akakubali mashtaka ya kuiba zaidi ya dola elfu 160 kutoka kwa benki na akatumikia kifungo cha mwaka mmoja unusu katika jela.

Wawili hao wanafurahia uhuru kwa sasa huku kesi dhidi yao ikiendelea. Wakili wao kwa jina Robert Rosenblatt alidhihirisha imani kwamba wataibuka washindi hatimaye.

Website |  + posts
Share This Article