Bondia wa kike wa India Saweety Boora amegonga vichwa vya habari kwa sababu zisizo za kuridhisha. Hii ni baada ya mshindi huyo wa nishani ya dhahabu katika mashindano ya ulimwengu kumpiga mume wake katika kikao cha talaka.
Saweety Boora na mume wake Deepak Hooda ambaye ni mchezaji Kabaddi na watu wengine walionekana kwenye video wakiwa kwenye kikao hicho katika kituo cha polisi cha Hisar.
Ghafla Boora ananyanyuka alipokuwa ameketi mkabala na Hooda na kuanza kumpiga.Kesi ya talaka ya wanamichezo hao tajika nchini India inafuatiliwa sana na wengi ndani na nje ya India.
Awali sababu ya wawili hao kutaka kutengana haikuwa wazi lakini Boora katika mkutano na wanahabari Machi 23, 2025 alifichia kwamba aligundua kwamba mume wake anapendelea sana mahusiano na wanaume wenzake.
Huku akibubujikwa na machozi, Boora aliambia wanahabari kwamba ana ushahidi tosha wa kuthibitisha madai dhidi ya mume wake akiongeza kwamba alikuwa pia akimdhulumu kimwili na kimawazo.
Hooda kwa upande mwingine alidai kwamba mke wake alimotishwa na mali aliyonayo kutafuta talaka ili wagawane mali, madai aliyokanusha vikali Boora.
Boora alisema alipokutana na Hooda kwa mara ya kwanza mwaka 2015 hakuwa na lolote ilhali yeye alikuwa tayari ameshinda medali kadhaa kutokana na mashindano ya ndondi.
“Ningekuwa nataka mali yake ningekubali kuwa naye nilipomkuta?” alishangaa Boora akiongeza kusema kwamba Hooda alipopata pesa nyingi kutokana na ligi ya Kabaddi mwaka 2016, aliweka pesa zote kwenye akaunti yake ya benki kama njia ya kukwepa kulipa ushuru.
“Alitoa pesa zake zote baada ya mimi kulipa ushuru.” alielezea bondia huyo nyota wa India. Inasubiriwa sasa kuona jinsi kesi hiyo ya talaka itakamilika.