Saudi Arabia imehimizwa kubatilisha vikwazo vya usafiri na utoaji wa viza dhidi ya raia wa Kenya, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Kupitia kwa taarifa ya kidiplomasia kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imesema vikwazo hivyo vitahujumu usafiri wa hija, ajira, elimu na biashara kati ya nchi hizo mbili.
kulingana na Wizara ya mambo ya Nje ya Kenya, taifa hili limefanikiwa kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo, huku waathiriwa wote wakitambuliwa.
“Huku Kenya ikitambua haki ya Ufalme wa Saudi Arabia kutekeleza mikakati ya kiafya kuambatana na sheria zake za kuwalinda wananchi wake, hatua zilizochukuliwa dhidi ya Kenya haziungwi mkono ushahidi wa kisayansi kuhusu hali ya afya nchini Kenya,” ilisema taarifa ya wizara hiyo.
Aidha, wizara hiyo ilitaja tathmini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwamba mlipuko wa ugonjwa huo ulidhibitiwa, huku shirika hilo likishauri dhidi ya kuwekwa kwa vikwazo vya usafiri na kibiashara.
Serikali imesema itawasiliana na kituo cha Kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika (Africa CDC), ikwa ushirikiano na mataifa mengine yaliyoathiriwa, ikionya kwamba vikwazo ambavyo hazina ushahidi wa kisayansi, ni ubaguzi dhidi ya mataifa ya Afrika.
Kenya imesema iko tayari kutoa taarifa za kiufundi kuhusu ugonjwa wa Ebola kwa Halmashauri ya Afya ya Umma ya Saudi Arabia.