Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani Ukraine

Marion Bosire
2 Min Read

Saudi Arabia inajiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa mazungumzo ya kutafuta amani nchini Ukraine. Mkutano huo utatathmini mpango wa Rais Volodymyr Zelenskyy wa kurejesha amani katika nchi yake hata ingawa uvamizi wa Urusi bado unaendelea.

Mkuu wa wafanyakazi katika serikali ya Zelenskyy Andriy Yermak ndiye alitangaza haya jana Jumapili akisema viongozi kutoka nchi mbalimbali wanapangiwa kuhudhuria mkutano huo. Lakini hakufichua wakati mkutano huo utaandaliwa na ni katika mji upi.

Kulingana na jarida la Wall Street, mazungumzo hayo yatafanyika Agosti 5 na 6 jijini Jeddah na nchi 30 zitawakilishwa.

Yermak alielezea kwamba mazungumzo hayo yatadurusu mpango wa amani wa Ukraine ambao una mambo 10 ya msingi ambayo utekelezaji wake utarejesha amani nchini Ukraine, mbali na kuzuia uvamizi siku zijazo.

Awali, Ukraine ilisema mpango wao wa amani unajumuisha kurejeshwa kwa himaya yake, kuondolewa kwa wanajeshi wa Urusi, kuachiliwa kwa mateka wote, kufikishwa mahakamani kwa waanzilishi wa uvamizi na Ukraine kuhakikishiwa usalama.

Yermak anaamini mpango wao wa mambo kumi msingi unafaa kuongoza mazungumzo na kwamba kila jambo kwenye orodha hiyo litajadiliwa kivyake.

Nchi na mashirika ambayo yamealikwa kwa mkutano huo wa Jeddah zinajumuisha Chile, Misri, Umoja wa Ulaya, Indonesia, Mexico, Poland, Uingereza, Marekani na Zambia, kulingana na jarida la Wall Street.

Urusi haijaalikwa kwa mkutano huo.

Website |  + posts
Share This Article