Sammy Douglas Waweru Kamau wa chama cha upinzani cha DCP,ndiye Mbunge mpya wa eneo bunge la Ol Kalou, baada ya kumbwaga Muchina Nyaga wa UDA, kwenye uchaguzi mdogo ulioandaliwa siku ya Alhamisi.
Waweru ametangazwa mshindi na msimamizi wa uchaguzi Antony Njiraine, kwa kuzoa kura 35,440, huku Muchina akiambulia kura 5,450.
Wilson Mwaniki wa chama cha Jubilee aliambulia kura 198,naye Stephen Waithaka, akipata kura 103, katika kinyang’anyiro kilichowashirikisha waaniaji tisa.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa chama cha DCP chake aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua tangu kibuniwe.
Idadi ndogo ya wapiga kura ikiwa chini ya asilimia 60 ilijitokeza kushiriki zoezi hilo la Kidemokrasia.
Aidha,visa kadhaa vya uhuni viliripotiwa siku ya uchaguzi huo ambao pia ulighubikwa na madai ya utoaji hongo kwa wapiga kura.
Kiti hicho kiliachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge David Njuguna Kiaraho,Machi 29, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 62,akipokea matibabu katika ikulu ya Nairobi.