Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,jana alikutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin,katika siku ya kwanza ya ziara rasmi huku wakijadiliana kuhusu ubia wa mataifa hayo mawili.
Dkt. Samia alisema ana matumaini kuwa ziara yake itaimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, hatua itakayochochea maendeleo.
Kwa upande wake, Rais Putin alisema Tanzania na Urusi, zimeendelea kuwa na uhusiano na ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo madini na nishati, akieleza kufurahishwa na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Rais Samia yupo nchini Urusi kwa ziara ya siku tatu hadi Juni 5, ambapo anatarajiwa kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha RUDN, taasisi yenye wanafunzi wengi wa Kitanzania.
Ziara ya Samia nchini Urusi ni ya pili kwa Rais wa Tanzania, tangu Hayati Julius Nyerere,alipozuru taifa hilo mwaka 1969.