Patrick Salvado Idringi amefichua kuwa atakapostaafu kutoka kwenye uchekeshaji, ana mpango wa kujitosa kikamilifu kwenye kilimo, jambo ambalo amekuwa akilifanya kwa kiwango cha chini kwa miaka mingi.
Akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika tasnia ya ucheshi nchini Uganda, Salvado anasema bado ana mengi ya kutoa, lakini tayari ameanza kufikiria kuhusu maisha baada ya umaarufu.
“Napenda kilimo na ninakifanya kimya kimya, lakini nafikiri nikistaafu, hicho ndicho nitakachokifanya,” alisema.
Mchekeshaji huyo pia alizungumzia kuhusu maisha ya kifamilia nje ya jukwaa, akifichua kuwa kwa sasa analea watoto peke yake tangu mkewe alipoenda kuishi Canada.
Salvado alikiri kuwa kulea watoto peke yake kuna changamoto, lakini uthabiti wa kifedha unasaidia kufanya mambo kuwa rahisi.
“Watoto wananisumbua, lakini kwa bahati nzuri nina hela, kwa hiyo maisha yanakuwa rahisi. Mke wangu ameridhika. Anajua ana mwanaume anayempenda, kwa hiyo hahangaikii sana kuhudu umbali kati yetu.”
Patrick “Salvado” Idringi ambaye sasa ana umri wa miaka 40, amekuwa kwenye tasnia ya ucheshi nchini Uganda tangu mwaka 2009. Pia anajihusisha na utangazaji wa redio pamoja na uigizaji wa filamu.