Mshambulizi wa Liverpool Mohamed Salah ametoa wito wa kusitishwa kwa vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza baina ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas.
Mshambulizi huyo wa Misri aliyasema hayo kupitia ujumbe wa video jana Jumatano baada ya kukashifiwa vikali nchini mwao kwa kutosema lolote kuhusiana na vita hivyo.
Salah ametaka pia misaada ya kibinadamu kuruhusiwa kutolewa kwa walioathirika na vita katika Ukanda wa Gaza.
Kulingana na Wizara ya Afya, Wapalestina 3,478 wameuawa na wengine 12,065 kujeruhiwa katika ukanda huo kutokana na vita hivyo.
Wafuasi wa Salah hususan nchini Misri, walianzisha kampeini ya mtandaoni mapema wiki hii kumtaka mchezaji huyo kulaani mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina, huku baadhi yao wakijiondoa kumfuatilia katika mitandao ya kijamii.