Sakaja apuuzilia mbali madai ya kumbandua mamlakani

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja, amepuuzilia mbali madai kwamba kuna njama ya kumbandua mamlakani.

Sakaja alisema huo ni uvumi na kwamba serikali yake imejitolea kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wakazi wa kaunti hiyo.

Akizungumza alipozindua awamu ya tatu ya kutoa lishe shuleni almaarufu ‘Dishi na County’ katika mtaa wa Umoja siku ya Jumatatu, Sakaja alitaja madai hayo kuwa kizuizi katika utekelezaji majukumu yake.

“Tumejenga vyumba 17 vya kupikia katika kaunti ndogo 17. Hatutapumbazwa na wapinzani wetu. Lengo letu ni kutekeleza tuliloahidi,” alisema Sakaja.

“Tuko na jukumu la kutekeleza, hatuna wakati wa kupoteza, hatuna wakati wa wanaoeneza uvumi. Lengo letu kuu ni kuwahudumia wakazi wa Nairobi sio kujihusisha na uvumi,” aliongeza Gavana huyo.

Wakati huo huo, Gavana huyo alipuuzilia mbali madai kwamba alifurushwa kutoka kwa ndege ya Rais iliyokuwa ikielekea China, akisema hakuwa ndani ya ndege hiyo.

Sakaja alidokeza kuwa alikuwa akishughulikia ratiba yake na wala hakutarajiwa kusafiri nje ya nchi.

“Ni ndege ipi watu wanazungumza kuihusu? Niliratibiwa kuwa Umoja na wala sio China. Huo ni uvumi tu,” alisema Gavana Sakaja.

Alitangaza kuwa atapanua mpango wa Dishi na kaunti, kuhakikisha wanafunzi wote katika kaunti ya Nairobi wananufaika na mpango huo.

Share This Article