Safari ya kihistoria: Kutoka Chongqing hadi Paris kwa skuta

Katika siku 55, Gu Chuang, mwenye miaka 26, alikamilisha safari ya kilomita 15,237 kupitia nchi 17, akithibitisha uwezo wa binadamu na ubora wa bidhaa za China.

KBC Digital
5 Min Read

Chongqing – Siku 55, nchi 17, kilomita 15,237, skuta moja. Gu Chuang, kijana mwenye umri wa miaka 26 kutoka Chongqing, amekamilisha safari ya kipekee barani Ulaya na Asia kwa kutumia skuta ya kichina, akipima mipaka ya uwezo wa binadamu na mashine.

“Nimefanikiwa! Nimeendesha skuta yangu yenye nambari za Chongqing kutoka China hadi Ufaransa!” alitangaza chini ya mwanga wa usiku katika Mnara wa Eiffel, akifanikisha nusu ya safari yake ya takriban kilomita 30,000 kwenda na kurudi. Safari yake, aliyoiweka mtandaoni, imepongezwa kwa ujasiri na kuibua hamu kuhusu gharama.

“Inaweza kuonekana jambo la ajabu, lakini ukithubutu kuota, daima kuna njia,” aliandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya kufika Paris. “Ukweli wa mambo maishani ni kwamba maisha yamejaa hali ya kutokujulikana.”

Kutoka Afrika Mashariki hadi Ulaya na Asia

Gu ni msafiri mwenye shauku, na mapenzi yake ya safari ndefu yalianza akiwa na miaka 16, alipoendesha baiskeli peke yake hadi Lhasa. Jeraha la goti alipokuwa jeshini lilionekana kuua ndoto zake za kuendesha baiskeli, lakini mnamo 2020 alihamia pikipiki. Katika miaka mitano tu, amesafiri Xinjiang na Xizang nchini China, na hata kutembelea nchi nne za Afrika Mashariki mapema mwaka huu.

Kwa safari yake ya Ulaya na Asia, alichagua skuta ya kichina iliyofanyiwa marekebisho, iliyomgharimu yuan 16,000 (takribani dola 2,227 za Marekani), badala ya pikipiki kubwa na za bei ghali zinazojulikana kwa safari ndefu.

“Ni rahisi zaidi kwa safari ndefu kuliko watu wanavyodhani,” alisema.

Ili kuokoa muda, Gu alisafirisha skuta yake kutoka Chongqing hadi Bandari ya Horgos huko Xinjiang kwa yuan 1,250, na kuanza safari yake tarehe 15 Juni. Iliyochorwa rangi nyekundu ya China, ikiwa na maandishi ya Kichina “Chuang” (jina lake la kwanza, linalomaanisha pia “kuthubutu”) pamoja na tai, na bendera ya China ikipepea, skuta yake ilikuwa na ujumbe mmoja: “Ukiwa unaendesha nje ya nchi, endesha kichina. Nilikuwa nataka dunia iione ubora wa bidhaa za China.”

Mataifa 17

Kazakhstan ilikuwa kituo chake cha kwanza, ambako aliweka rekodi ya siku yake ndefu zaidi ambayo ilikuyuwa kilomita 700 ndani ya saa 10, kwa sababu ya barabara laini na mandhari wazi. Alipitia mataifa ya Urusi, Georgia, Türkiye, Kroatia, Italia, Ujerumani, Austria, na zaidi, akafika Ufaransa tarehe 7 Agosti. Safari ya kurudi ikafuata njia tofauti ya kilomita 15,000, na gharama jumla zikikadiriwa kufikia yuan 80,000.

Kando na njia, alitembelea sanamu kubwa ya Kisovyeti “The Motherland Calls” huko Volgograd, mji wa Dubrovnik nchini Kroatia uliotumika kurekodi filamu ya Game of Thrones, na mandhari ya puto za hewani nchini Türkiye. Katika Ziwa Sevan nchini Georgia, alisimama na kusema: “Zuri sana, kama Ziwa Sayram kule Xinjiang.”

Sanduku la nyuma la skuta yake sasa lina ramani iliyochapishwa ya njia yake, ikiwavutia watu na waendesha pikipiki wengine. Nchini Armenia, mwanapikipiki kutoka Dubai alimwambia mara kadhaa: “Pikipiki za kichina ndizo bora zaidi duniani.”

Majeraha, changamoto na upweke

Safari haikuwa rahisi. Mvua kubwa nchini Urusi iligeuza barabara ya vumbi kuwa tope, na kusababisha aanguke mara nne na kuumia mbavu kabla ya baba na mwana kumvuta hadi usalama. Nchini Georgia, alipitia barabara za milima zenye ukungu mzito, miteremko mikali na mwonekano chini ya mita tano, akaanguka tena na kujeruhi mguu.

Hata hivyo, hakuwahi kufikiria kufa moyo au kuacha.

“Kuendesha pikipiki ni furaha iliyoambatana na hatari. Usalama ni wa kwanza, na lazima uendeshe kulingana na uwezo wako,” alisema.

Gu husafiri kwa urahisi, hupika barabarani na mara chache hujiburudisha kwa ladha ya nyumbani kwa kutumia viungo vya hotpot na tambi, akiwashirikisha wenyeji harufu na picha za hotpot ya Chongqing.

Lakini pia safari imekuwa ya upweke. “Upweke sana,” alikiri bila kusita. “Lakini shida inaongeza uzoefu. Miaka kumi iliyopita, singewahi kufikiria kuona machweo ya Siberia au kufika Ufaransa kwa skuta.”

Alipokutana na msichana wa Kijerumani mwenye umri wa miaka 19 nchini Türkiye aliyekuwa akipanda lifti kutoka China kurudi Ujerumani, alithibitisha imani yake: “Maisha yana uwezekano usio na mwisho. Unachohitaji kuanza si pesa—ni ujasiri.”

Gu hajafunga milango ya kuendesha Amerika Kaskazini au Kusini siku zijazo. Kwa sasa, anazingatia kurudi nyumbani salama, akiwa na skuta inayobeba mwendeshaji, Pamoja na hadithi ambayo tayari imewapa maelfu msukumo.

Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na ichongqing.info

KBC Digital
+ posts
Share This Article