Viongozi wa EAC waunga mkono azima ya Raila kugombea uenyekiti wa AUC

Martin Mwanje
2 Min Read
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC wanaunga mkono azima ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC. 
Akizungumza mjini Kisii, Raila ameelezea imani yake kuwa serikali za Afrika zitaunga mkono juhudi zake za kugombea wadhifa huo akiongeza kuwa ameanza kuona dalili chanya.
“Siku ya Jumatatu, nilikutana na Rais William Ruto na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na kuwataka kuunga mkono azima yangu. Wote walikubali kuniunga mkono,” alisema Raila wakati akiwa mjini Marani katika eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini.
“Isitoshe, Rais Museveni alisema ni yeye atakayenipendekeza kwa wadhifa huo”, aliongeza Raila.
Waziri huyo Mkuu wa zamani alisema ataelekea mjini Kigali nchini Rwanda ambako atatafuta uungwaji mkono wa Rais Paul Kagame na wa serikali yake.
“Nimezungumza na Rais Salva Kirr wa Sudan Kusini na amekubali kuniunga mkono. Hata Mama Suluhu wa Tanzania amesema ataniunga mkono”.
Kadhalika, Raila alidokeza kuwa alifanya mazungumzo na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye pia aliahidi kumuunga mkono kuwania wadhifa huo.”
“Nitazungumza na viongozi wote wa bara la Afrika kutafuta uungwaji mkono wao. Niko tayari kugombea wadhifa huo na yeyote atakayegombea wadhifa huo, niko tayari”.
Raila analenga kumrithi Moussa Faki Mahamat kutoka Chad ambaye muda wake wa kuhudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika unaelekea kukamilika.
Share This Article