Sabina Chege apuuzilia mbali wapinzani

Marion Bosire
2 Min Read

Mwenyekiti wa chama cha Jubilee Sabina Chege amepuuzilia mbali wanaompinga akisema anatosha kuongoza chama hicho cha Jubilee kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta.

Chege ambaye alizungumza huko Nairagie-Enkare kwenye sherehe ya shukrani ya mwakilishi wa wadi ya Keekonyokie Lemiso Kimiti wa chama cha Jubilee alisema kwamba chama hicho kinalenga kuwa na wabunge wasiopungua 100 kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Chege amekuwa akikabiliana na aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni kuhusu atakayechukua uongozi wa chama baada ya kuondoka kwa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.

Mwakilishi huyo wa zamani wa kaunti ya Murang’a bungeni na ambaye sasa ni mbunge mteule alifichia kwamba chama cha Jubilee kilichagua kuingia kwenye muungano wa Kenya Kwanza kwa sababu hawakuwa tayari kujiunga na maandamano ya kuharibu yaliyopangwa na muungano wa Azimio La Umoja One Kenya.

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na gavana Patrick Ole Ntutu, aliyekuwa gavana Samuel Ole Tunai na mbunge wa Narok Mashariki Lemanken Aramat.

Aramat wa chama cha UDA alisisitiza kwamba hakukua na ombwe katika uongozi wa chama cha Jubilee kwani Sabina Chege yuko pale.

Ntutu alitumia fursa hiyo kutetea ajenda ya serikali yake ya maendeleo na umoja.

Hii ni baada ya mwakilishi wa wadi ya Kimiti kumlaumu gavana kwa kile alichokitaja kuwa kubagua watu wa wadi yake katika kugawa nafasi za ajira.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *