Serikali ya Rwanda imetangaza kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ubelgiji mara moja.
Kwenye taarifa, Kigali inasema iliitarifu serikali ya Ubelgiji juu ya uamuzi huo leo Jumatatu.
Rwanda inasema imechukua uamuzi huo baada kuzingatia kwa makini vigezo mbalimbali, vyote vinavyohusiana na juhudi za kikoloni za Ubelgiji za kuendelea kuikandamiza nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
“Ubelgiji imeendelea kuidunisha Rwanda, kabla na baada ya mgogoro unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo Ubelgiji ina wajibu mkubwa wa kihistoria na vurugu, hasa katika kuchukua msimamo wa kuipinga Rwanda,” ilisema Rwanda katika taarifa.
“Leo, ni bayana Ubelgiji imeegemea upande mmoja katika mgogoro wa kimaeneo na inaendelea na ukusanyaji wa kimfumo dhidi ya Rwanda katika makongamano mbalimbali, ikitumia uongo na hila kupata maoni ya kiusahama na yasiyokuwa ya haki dhidi ya Rwanda, katika jaribio la kusababisha ukosefu wa uthabiti nchini Rwanda na katika eneo hili,” iliongeza taarifa hiyo.
Kutokana na hatua hiyo, wanadiplomasia wote wa Ubelgiji wametakiwa kuondoka nchini Rwanda ndani ya saa 48 zijazo.
Aidha, Rwanda inasema itahakikisha ulinzi wa majengo na mali ya ubalozi wa Ubelgiji jijini Kigali kwa mujibu wa mkataba wa Vienna.