Rais William Ruto amesema kuwa maafisa wa polisi walijitahidi kadri ya uwezo wao kudhibiti maandamano ya kitaifa ya vijana wa Gen Z.
Vijana hao walifanya maandamano katika miji mbalimbali nchini kupingwa Mswada wa Fedha 2024 ambao kwa sasa umefutiliwa mbali.
Akizungumza Jumapili jioni kwenye Ikulu ya Nairobi, wakati wa mahojiano na wanahabari, Rais amekanusha kuwepo kwa mauaji ya kiholela yaliyotekelezwa na maafisa wa polisi wakati wa kukabiliana na waandamanaji.
Pia amekanusha kuwepo kwa visa vya polisi kuwanasa kiholela Wakenya kuhusiana na maandamano hayo.
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini yameisuta vikali serikali kwa kuwakandamiza waandamanaji, ambayo imesababisha vifo vya angalau watu 20 na mamia ya wengine kujeruhiwa.
Aidha serikali imeshutumiwa kwa mwenendo wake wa kuwateka nyara watu wanaoshukiwa kuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali.