Utawala wa Kenya Kwanza umeapa kuangamiza zimwi la ufisadi nchini.
Rais William Ruto anasema kuukubalia uovu kuenea kutakuwa mwiba kwa utekelezaji wa manifesto ya serikali yake.
“Hatutaruhusu ufisadi na wizi na ukora kuharibu nafasi yetu ya kutekeleza manifesto na kuhakikisha kwamba pesa za umma zinatumika katika transformation ya taifa letu la Kenya. Hiyo haitafanyika,” aliapa Rais Ruto wakati akihutubia Baraza la Kitaifa la Uongozi wa chama UDA katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.
“Kwa wakora wote, na wezi na wale wa ufisadi, mambo yao ni matatu: wahame Kenya, waende jela au waende mbinguni.”
Rais Ruto akitumia fura hiyo kuelezea imani kuwa serikali ya Kenya Kwanza imemakinika katika kulihudumia taifa hili.
“Mimi nataka niwahakikishie kuwa hii serikali itabadilisha taifa la Kenya. Sina shaka akilini mwangu kuwa huu ndio utawala ambao unaenda kubadilisha Kenya kuwa bora zaidi,” aliahidi Rais Ruto.
Ahadi zake zikija wakati ambapo kanisa la Kiangiliana nchini, ACK limeukosoa utawala wa Kenya Kwanza kwa kuwa na hulka ya kusema mengi bila vitendo.
Kanisa hilo chini ya Askofu Jackson Ole Sapit sasa linaitaka serikali ya Rais Ruto kuachana na longalonga nyingi na kutimiza ahadi ilizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.